Unachohitaji kujua kuhusu Medabon

Matumizi, Maudhi, Kipimo, na Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara

Medabon ni jina la vidonge vya kutoa mimba vinavyo patikana nchini Kenya, Uganda na Tanzania. Vidonge hivi hujumuisha aina mbili za dawa za kutolea mimba ambazo ni salama na zinafaa kwa kutolea mimba.

Maelezo ya Bidhaa

Medabon hujumuisha dawa mbili ambazo hutumika kutoa mimba: Mifepristone na Misoprostol. Mifepristone na Misoprostol ni majina ya kawaida ya dawa hizi, lakini wakati mwingine hutajwa kwa majina ya chapa zao. Dawa hizi hutumiwa kwa pamoja ili kutoa mimba na kila dawa ina kazi tofauti katika kufanikisha utoaji mimba.

 • MIFEPRISTONE. Mifepristone ni dawa ya kwanza unayopaswa kutumia wakati wa utoaji mimba. Mifepristone hufanya kazi kwa kuzuia homoni inayoitwa progesterone, ambayo ni muhimu katika kuendeleza mimba. Progesterone inapo zuiliwa, hupelekea kuvunjwavunjwa kwa utando wa mfuko wa uzazi na kusitisha ukuaji wa mimba.
 • MISOPROSTOL. Misoprostol ni dawa ya pili unayopaswa kutumia wakati wa utoaji mimba. Dawa hii hutumika mara baada ya Mifepristone kuzuia mimba kuendelea. Misoprostol husafisha mfuko wa uzazi na mabaki hutolewa nje (1).

Faida za Medabon

Medabon ni njia salama na yenye ufanisi mkubwa inayo tumika kutoa mimba. Pia, ni njia maarufu sana na hupendekezwa na wataalamu wa matibabu kwa watu wanaotaka kutoa mimba.

Kwa bahati mbaya, watu takribani milioni 21 hufanya utoaji mimba usio salama na haramu kila mwaka. Utoaji mimba usio salama hufanywa katika mazingira hatarishi, na hufanywa na wataalamu wasiothibitishwa au kutumia njia zisizofaa. Utoaji mimba usio salama husababisha vifo vya takriban wanawake 50,000 kila mwaka (2). Hata hivyo, Medabon ni njia salama ya kutoa mimba ambayo kwa kawaida husababisha athari ndogo na za muda tu.

Medabon pia hukupa faragha na faraja linapokuja suala la kutoa mimba. Njia mbadala ya kutoa mimba ni kutumia wataalamu wa kliniki, ingawa hii nayo ni njia yenye ufanisi, lakini si kila mtu anaweza kuifikia kwa urahisi. Kwa kutumia Medabon, unaweza kutumia vidonge vya kutoa mimba kwa siri katika eneo unalopenda na haulazimiki kusafiri au kuomba msaada kama ilivyo kwa njia nyingine. Pia, kwa sababu njia hii inaweza kutumika hata ukiwa nyumbani, unaweza kuwa na faraja zaidi.

Ikitumiwa kwa usahihi, Medabon ni njia yenye ufanisi sana katika utoaji mimba (3).

Bei ya Medabon

Bei ya Medabon kwa kawaida huwa ndogo, lakini hili hutegemea eneo la kijiografia. Nchi huwa na sheria tofauti kuhusu utoaji mimba, na hii inaweza kuathiri bei ya dawa pia.

Jinsi ya kutumia Medabon

Kutumia Medabon kwa usahihi, anza kwa kumeza kidonge cha Mifepristone. Kidonge hiki hupatikana katika dozi ya mg 200. Kupitia kidonge hiki, utazuia homoni ya progesterone na kusitisha ukuaji wa mimba. Pia huandaa kizazi kuwa tayari kutoa mimba. Baada ya kutumia Mifepristone, subiri kwa saa 24-48 kabla ya kutumia Misoprostol. Vidonge vya Misoprostol huwa vinne ambavyo huwa na mcg 200. Huenda ukahitaji vidonge zaidi vya Misoprostol, kutegemea na umri wa mimba yako (5).

Nitarajie nini baada ya kutumia Medabon?

Medabon, ikitumika kwa usahihi, ni njia inayofaa sana ya utoaji mimba lakini matumizi ya vidonge hivi yanaweza kusababisha athari za muda mfupi ambazo ni pamoja na:

 • Maumivu ya tumbo,
 • Kutokwa na damu nyingi,
 • Kichefuchefu,
 • Kutapika,
 • Kuharisha,
 • Kutetemeka, na
 • Homa (6).

Dalili kama vile kutokwa na damu na maumivu ya tumbo ni za kawaida na zinatarajiwa, na kwa kawaida hutokea ndani ya saa 24. Maudhi haya yanaweza kufanana na hedhi nzito sana kwasababu mwili wako unatoa mimba na utando wa kizazi na vinaweza kutoka kama vipande vikubwa vya damu. Kwa kawaida maumivu ya tumbo hutokea ndani ya siku mbili za kwanza baada ya kumeza vidonge, lakini maumivu kiasi yanaweza kuendelea kwa muda kidogo, pia kutokwa na damu pamoja na matone kunaweza kuendelea kwa wiki kadhaa baadaye (7).

Je, nifanye nini kupunguza maudhi ya Medabon?

Kama tulivyo tangulia kusema, Medabon inaweza kusababisha maudhi mbalimbali ambayo huja kama matokeo ya utoaji mimba na kusafisha tumbo la uzazi. Ikiwa utapata maumivu na uchungu, unashauriwa kumeza ibuprofen. Unaweza kutumia vidonge viwili vya ibuprofen vyenye mg 400 dakika 30 kabla ya kumeza vidonge vya Misoprostol ili kuzuia baadhi ya maumivu yanayohusiana na vidonge vya kutoa mimba. Pia unaweza kutumia njia kama vile pedi za joto au waweza kuoga maji ya moto ili kupunguza maumivu(7).

Ni akina nani hawapaswi kutumia Medabon

Medabon haipaswi kutumiwa na watu wenye hali zifuatazo:

 • Wenye mimba iliyotunga nje ya kizazi,
 • Wanaotumia kifaa cha intrauterine (IUD),
 • Wenye anemia kali (upungufu wa damu),
 • Wenye matatizo ya kutokwa na damu au watu wanaotumia dawa za kuongeza damu, na
 • Wanaopata mzio pindi watumiapo Mifepristone au prostaglandini kama vile Misoprostol (8)(9).

Je, Medabon ina iliana na dawa nyingine?

Medabon hai ingiliani na dawa nyingi, ingawa kuna baadhi ya mazingira yanayoweza kupelekea ulazima wa kuingiliana na dawa nyingine. Dawa hii haishauriwi kwa watu wanaotumia dawa za muda mrefu za steroidi (prednisone, dexamethasone) au watumiaji wa vidonge vinavyoweza kupelekea kutokwa na damu (warfarin, heparin, n.k.). Medabon inaweza kuingiliana na dawa nyingine maalumu lakini dawa hizi hutofautiana kulingana na hitaji la mtumiaji.

Maswali Yanayoulizwa Mara kwa Mara

Ni nani anayeweza kutumia Medabon?

Medabon inaweza kutumika kutoa mimba yenye hadi wiki 13.

Nawezaje kupata Medabon?

Upatikanaji wa Medabon hutegemea eneo ulilopo. Inaweza kupatikana katika duka la dawa kwa maelekezo maalumu. Wasiliana na washauri wetu kupitia barua pepe au mazungumzo ya moja kwa moja nao watakusaidia kupata mtoa huduma wa kuaminika aliye karibu yako.

Hitimisho

Medabon ni njia salama na yenye ufanisi ya kutoa mimba inayowezesha kutoa mimba kwa faragha ukiwa nyumbani. Njia hii hujumuisha dawa mbili muhimu ambazo ni Mifepristone na Misoprostol ambazo zina kazi tofauti lakini zote ni muhimu katika mchakato wa kutoa mimba. Unaweza kupata maudhi ya muda mfupi, kama vile maumivu na kutokwa na damu kwa saa au siku chache baadaye. Ikiwa una shaka yoyote, waweza kuzungumza na mshauri wa safe2choose.

 1. “The Facts on Mifepristone.” Planned Parenthood, www.plannedparenthood.org/uploads/filer_public/42/8a/428ab2ad-3798-4e3d-8a9f-213203f0af65/191011-the-facts-on-mifepristone-d01.pdf. Accessed April 2023.
 2. “Facts are Important: Abortion is Healthcare.” ACOG, www.acog.org/advocacy/facts-are-important/abortion-is-healthcare. Accessed April 2023.
 3. “The Abortion Pill.” Planned Parenthood, www.plannedparenthood.org/learn/abortion/the-abortion-pill. Accessed April 2023.
 4. “Unwanted-Kit Strip of 5 Tablets.” PharmEasy, pharmeasy.in/online-medicine-order/unwanted-kit-tab-18194. Accessed April 2023.
 5. “Unwanted-Kit.” Apollo Pharmacy, www.apollopharmacy.in/medicine/unwanted-kit-tablet. Accessed April 2023.
 6. “Uses of Misoprostol in Obstetrics and Gynecology.” NIH, 2009, www.ncbi.nlm.nih.gov/pmc/articles/PMC2760893/. Accessed April 2023.
 7. “How Does the Abortion Pill Work?” Planned Parenthood, www.plannedparenthood.org/learn/abortion/the-abortion-pill/how-does-the-abortion-pill-work. Accessed April 2023.
 8. “Mifepristone.” NIH, 2022, www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK557612/#:~:text=Mifepristone%20is%20contraindicated%20in%20patients,hemorrhagic%20disorders%2C%20and%20severe%20anemia. Accessed April 2023.
 9. “Misoprostol.” NIH, 2022, www.ncbi.nlm.nih.gov/books/NBK539873/#:~:text=Misoprostol%20is%20contraindicated%20in%20those,adverse%20effects%20reported%20during%20pregnancy. Accessed April 2023.