Elimu ya jinsia na ngono kwa vijana inajumuisha na kulenga uhamazishaji na maelezo ya mfumo wa uzazi kubaleghe, magonjwa ya zinaa, mimba za ujana, uzuiaji mimba, majukumu ya kijinsia na dhana zinazoambatana zikiwemo dhuluma na udhalilishaji wa jinsia. Elimu na mawaidha haya yanakusudiwa kuongoza vijana kujifahamu na kufanya maamuzi bora wanaponawiri na kupata umakini wa mambo ya tahadhari na kinga kwa umri mdogo.
Hitaji Kuu La Uhamazishaji Katika Jumuia Ya Afrika Mashariki
Haja kuu imeshuhuduhiwa katika Bara la Afrika kuelimisha jamii kuhusu ngono na uhusiano wa kijinsia. Jambo hili limesisitizwa katika jumuiya ya Afrika Mashariki kwa sababu za maswala muhimu na ya dharura yaliyoorodeshwa:
- Takwimu za juu za Magonjwa ya zinaa na mimba ya ujana: kulingana na utafiti, idadi kubwa ya watu wanaoambukizwa magonjwa ya zinaa ni vijana walio na miaka 15-24. Mfano huu unakiwakilisha 41% ya jumla ya maambukizi nchini Kenya. Vile vile, wastani 23% ya vijana katika eneo hili wanapata mimba ya ujana.
- Uhasama kwa misingi ya kijinsia: tatizo hili limetajwa kuwakabili wanawake katika jamii hasa katika ujana hata kabla ya miaka 20. Elimu hii ni muhimu ili kuhamasisha vijana kuhusu haki zao na hatua za kuawalinda na kuwawezesha kujikinga na maswala ya kudhulumiwa na misingi ya kijinsia.
- Taaarifa potovu katika jamii: Mara nyingi imani na hekaya za kitamaduni husababisha habari zisizo sahihi kuhusu ngono. Maoni hayo yasiyo sahihi, yanayochochewa na ubaguzi na ukosefu wa habari sahihi, yanaathiri vibaya afya na maamuzi ya vijana. Elimu wazi, utamaduni nyeti, na ushahidi-msingi ni muhimu ili kushughulikia mapungufu haya na kusaidia maamuzi ya habari.
- Michakato na kuhusishwa katika mfumo wa elimu: washikadau na wahusika katika mifumo ya elimu wamesisitiza umuhimu wa kuhusisha maaarifa ya ngono na majukumu ya kijinsia katika ngazi mbali mbali ili kuwafaa vijana na kuwapa ujuzi wa maisha. Kwa sababu hii, ni muhimu kusisitiza malengo haya ili kuwafikia vijana katika maeneo tofauti. Hili hasa ni kwa ajili ya kumaliza sera potovu katika jamii.
- Unyogofu wa pambano la elimu: Licha ya hatua zilizofadhiliwa hadi sasa, maswala ya kijinsia, mimba ya ujana na kwa watoto, elimu ya unyumba na magonjwa ya zinaa hajawasilishwa vilivyo kwa vijana. Baadhi ya changamoto zikiwa ni asili za jamii, kuwafikia vijana na mitazamo ya kibinafsi.
Elimu Ya Ngono Na Dhana Husika
Elimu ya jinsia ni mfumo ya kuhamazisha vijana kwa kuwapa mafunzo, maelezo yaliyo na kweli kuhusu ngono, maumbile, jinsia na maarifa ya uhusiano kulingana na umri wao. Mawaidha haya ni muhimu katika kila ngazi ya kustawi kwa vijana ili kuwapa ujuzi na maadili ya mambo ya kutarajia hadi utu ukubwa. Ni muhimu kukazia dhana mbali mbali kuwapa fursa ya kuelewa mambo kadhaa yanayoweza kupotoshwa na asili za kijamii. Ongezeko la maradhi na mimba kwa vijana wadogo ni ushahidi tosha kuhitaji elimu hii kwa vijana.
Dhana muhimu katika elimu ya ngono
Mfumo Wa Uzazi Na Maumbile
Uzazi huzingatia kustawi kwa mtu na ukomavu katika maumbile na afya ya sehemu za uzazi. Kuzingatia ngazi tofauti katika maisha ya vijana na jinsia tofauti ni muhimu kwa kuwaelekeza matarajiwa tofauti na jinsi ya kukubali na kuitikia mabadiliko haya.
Uzazi Wa Mpango
Vijana ni nguzo katika jamii na uwezo wa kunawiri unategemea uwezo na utimamu wa akili na afya ili kufanikiwa katika familia na kwa jamii. Katika suala hilo, ni muhimu kuwaelimisha katika elimu ya afya na uzazi wa mpango kuepukana na kuathirika kimwili na akili kwa magonjwa ya zinaa, mimba ya ujana na mimba zisizotarajiwa.
Kundi la vijana limeonekana kuwekewa mkazo zaidi kwani linatajwa kuathiriwa zaidi na changamoto zitokanazo na kutozingatia elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwani takwimu zinaonyesha asilimia 43 ya watu wote wanaoishi na virusi vya ukimwi ni vijana, miongoni mwao asilimia 80 wakiwa ni vijana wa kike, na hivyo wapo kwenye hatari kubwa sana ya ustawi wa maisha yao.
Mahusiano Na Idhini
Elimu katika idhini, heshima na kusudi katika uhusiono ni jambo la kimsingi kwa vijana wanaokua. Fahamu ya mambo haya ikiwemo nafasi na haki zao katika uhusiano yana uhaba hasa katika jamii asili. Ukosefu huu unathibiti haja ya kuzingatia mafunzo haya na kuyaendeleza katika sehemu mbali mbali ili kuwasaidia vijana kudumisha uhusiano mwema na kutangamana.
Kudhibiti magonjwa ya zinaa
Kufadhili na kueneza maarifa kuhusu magonjwa ya zinaa na ukimwi ni mojawapo ya nguzo muhimu katika elimu uzazi na ngono. Elimu hii itasaidia vijana kupunguza na kujikinga kuambukizwa magonjwa haya.
Umri Mwafaka Kwa Elimu Ya Uzazi Na Dhana Zake
Ni muhimu kuanzisha elimu ya maumbile, uzazi na wajibu wa jinsia mapema kwa watoto kadri ya umri wao. Kuwasilishwa huku ni msingi muhimu unaowapa vijana mafunzo muhimu ili kujielewa na kujichunga wanapokua. Maelezo tofauti yanaweza kuwasilishwa ifuatavyo:
Umri 3-5: Mafunzo ya msingi na usiri wa maumbile
Umri huu umeegezwa katika ufahamu wa kwanza na haja ya kujielewa maumbile. Ni muhimu kuzingatia mfumo wa maumbile na maelezo kadri ya sehemu za siri. Hili ni muhimu katika msingi wa dhana ya usiri, mipaka katika kutangamana na heshima kwa watu wengine. Nguzo kuu katika masomo haya ni kuwa na afya bora na usalama wa mwili.
Umri 6-9: Msingi wa ujana na mfumo wa uzazi
Ujana na mabadiliko ya kimaumbile huanza katika umri huu. Ni muhimu kuweka msingi wa kuelewa mabadiliko yanayoanza na kueleza mfumo wa maumbile na heshima hasa kutoka kwa watu wengine. Hoja ya kuzingatia kwa umri huu ni kwamba kijana anapokuwa usalama wake kulingana na mwili na kutangamana ni muhimu.
Umri 10 Kuendelea(Ujana): Elimu ya kina ya ujana, Uhusiano na idhini
Umri huu huwasilisha ujana, mabadiliko katika mfumo wa maumbile, hisia na haja. Katika kuelekeza vijana, mawaidha ya kuwasaidia kuelewa kua kwao kwa hisia na mfumo wa uzazi huwa mwongozo katika umri huu. Elimu hii iwe nguzo katika kufanya maamuzi ya uhusiano, kuungana na wengine kwenye mtandao. Kwa kuwa hisia na haja hustawi katika hili kundi, mafunzo ya uzazi na mpango wa uzazi, magonjwa na zinaa ni muhimu yatiliwe maanani.
Kuimarisha Mfumo Wa Elimu Ya Kunawiri Na Jinsia
Mwongozo kwa vijana katika miaka ya kukomaa hufaidi afya yao kimaumbile na mawazo kwa njia ya kuwaepusha kutoka kwa madhara ya ngono na uzazi usiotarajiwa. Kuimarisha mifumo ya elimu ni sehemu ya nguzo katika kufikia jamii na mawaidha haya ili kuwapa msingi mwafaka kuchagua yanayofaa. Jambo hili linahitaji washikadau tofauti wakiwemo wazazi, shule, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kushirikiana katika jamii. Nafasi na majukumu yao yameratibishwa ifuatavyo:
Serikali
Kutengeneza na kutekeleza mifumo: serikali ina wajibu mkuu katika usinduzi wa miundo misingi na mifumo kuwakilisha ufaafu wa elimu katika jamii. Mashirika ya kiserikali huongoza kuchapisha, kuimarisha na kusambaza sera za afya na mipango ya afya katika nchi.
Kuwekeza katika elimu: serikali ina wajibu ya kuwekeza fedha kusaidia kutengeneza mifumo ya elimu, kufadhili mafunzo kwa walimu na kusambaza rasilimali hizi katika jamii ili kuwafikia na kuwafaidi vijana wote.
Mashirika yasiyo ya kiserikali
Mashirika binafsi ni uti wa mifumo ya elimu na utekelezaji wa miundo misingi mbali mbali hasa katika jamii zilizo vijijini. Ufadhili wa mashirika haya hufaidi katika kufikia na kutangamana na watu ili kuwasilisha elimu ya uzazi hata pale serikali haijafanikiwa.
Mashirika haya hufaidi katika ufahamu wa kina na utekelezaji wa elimu ya uzazi na jinsia. Mashirika kama WHO na UN hufadhili miongozo ya elimu na kusaidia kuelekeza watu kutoka kasumba potovu.
Shule
Shule zinawajibika katika mafunzo ya vijana kuanzia utotoni hadi ujana kuhusiana na mfumo wa uzazi, maumbile, ngono na magonjwa ya zinaa. Kulingana na umri wa mwanafunzi, shule zikiongozwa na serikali huandaa masomo yayofaa na kuyajumuisha katika mitaala ya elimu.
Kuwaidhinisha na kufunza walimu- Wakufunzi hupewa mafunzo na kufadhiliwa na shule ili kuwapa wanafunzi masomo na ujuzi kulingana na mtaala. Hili ni muhimu kuwasilisha mafunzo maswala ya uzazi, ngono na magonjwa ya zinaa kwa vijana.
Wazazi
Mafunzo ya kwanza hutekelezwa na wazazi kwa mtoto anapokua. Ni jukumu la mzazi kufadhili mazingira ambayo kijana anaweza zungumza na kuelezwa kwa kina mambo yanayomhusu. Mzazi huifadhi uhusiano wake na mtoto ili awe na mwelekezi bora na mwaminifu.
Msaada wa mzazi pia ni kufadhili maelezo muhimu kwa mafunzo anayopata katika mifumo tofauti. Mzazi atawajibika kwa uhusiano wa mtoto na kuhakikisha anaelewa na kufanya chaguzi zinazofaa akiwa umri tegemezi.
Ratiba Na Mifumo Muhimu Iliyofanikishwa Katika Mwongozo Wa Elimu Kwa Vijana
Kufadhili na kuimarisha elimu ya zinaa kwa vijana hasa katika jumuiya ya Afrika mashariki kunahitaji ushirikiano wa mashirika tofauti ili kuwafikia vijana katika sehemu tofauti. Kati ya mashirika yanayofanikisha ujumbe huu ni:
Comprehensive Sexuality Education (CSE) Integration- Kenya
Mfumo huu umekuwa thabiti katika kuwasilisha masomo ya ujana na uzazi katika mitaala ya elimu shuleni kama wazo la lazima wanafunzi wote kufunzwa kuhusu jinsia, uzazi na magonjwa ya zinaa na kuyazuia. Vilevile shirika hili limekuwa kipau mbele katika kuelekeza walimu.
National Sexuality Education Framework
Mfumo wa kitaifa Uganda unaohusika na kuandaa na kutekeleza mitaala ya elimu ambayo inatekelezwa shuleni kuhusu jinsia. Pia, inahakikisha kwanza mitaala na ufadhili wa walimu katika masomo haya inafanywa na chopo la elimu nchini.
Education Plus Initiative
Mfumo huu unashirikisha nchi zote bara Africa katika kujitolea kuangamiza magonjwa ya zinaa na kukabili ukimwi barani kwa kutoa mafunzo kwa jamii. Katika maono haya, shirika hili linazingatia elimu kwa wasichana na ufadhili wa kupunguza maambukizi ya Ukimwi na magonjwa ya zinaa.
Hatua Kwa Utendaji (Hutau Sasa!!)
Kwa miaka mingi, hatua za kutekeleza elimu ya jinsia kama haki ya kila mmoja katika jamii limezingatiwa lakini kundi kubwa la vijana halijafikiwa kwa ufaafu. Kuangazia jumuiya ya Afrika Mashariki, vijana wengi wamekumbwa na janga la Ukimwi, magonjwa ya zinaa, ndoa za ujana na uhasama wa kijinsia kutokana na kukosa elimu na mafunzo haya. Kulingana na UNAIDS wastani wa maambukizi mapya ya VVU mwaka wa 2023, milioni 1.3 na takriban nusu ya walioambukizwa wanaishi mashariki na kusini mwa Afrika (35%) huku magharibi na Afrika ya kati wakiwa na maambukizi kwa asilimia 15%. Ni muhimu pia kuangaza ya kwamba asili za kijamii zimedhoofisha juhudi zilizowekwa kuelimisha vijana.
Mambo kadhaa yametiliwa mkazo katika sehemu hii ya kuelimisha vijana hasa katika shule. Ingawaje, tafiti zinaonyesha kwamba masomo haya hayana kina kinachofaa kuwaelimisha wanafunzi na etekelezaji wa mitaala haujafanywa kulingana na haja. Vile vile, kuna kikundi kikubwa cha vijana hakijafikiwa na masomo haya kwa uchahe wa miundo misingi na wafadhili. Muhimu katika utekelezaji wa nguzo hii ni ufadhili wa vifaa vya kujikinga ambavyo havijapatikana kwa maeneo ya jumuiya kutokana na shida mbali mbali.
Muda ni sasa. Ni muhimu sasa kuangalia mifumo iliyopeanwa, ufadhili, utendakazi na utekezaji wa elimu hii kwa vijana ili kuwafikia wote katika jamii. Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) inakiri mwanya katika kuwafikia vijana katika maswala haya almradi hitaji la ufumbuzi wa haraka. Hili ni jambo linalohitaji ushirikiano wa mashirika, serikali na juhudi binafsi ili kutekeleza mafunzo haya kwa afya ya vijana na jamii kuthibiti afya ya kijinsia, uzazi na maumbile.
Maswali Ya Mara Kwa Mara
Q1: Elimu ya jinsia huwafaidi vipi vijana?
Elimu ya jinsia, hasa inayosisitizwa kwa kina, huwapa vijana mwongozo katika maswala ya jinsia, magonjwa ya zinaa, kunawiri na mambo yanayotarajiwa ukikua, afya ya uzazi na maumbile. Kwa ujumla, mawaidha haya huwaelekeza vijana kukua na kuwaepusha na athari za uhusiano usio wa idhini. Kupitia mafunzo haya, vijana wanaweza kufanya maamuzi kwa afya na maisha yao.
Q2: Elimu ya jinsia inasaidiaje kupunguza uzazi wa ujana?
Katika mtaala na mfumo wa elimu ya jinsia, huelekezwa kujihini ya nngono hadi umri unaofaa, kuhusu njia mwafaka za kujikinga endapo wanashiriki tendo la ndoa kama kutumia mipira. Vilevile, vijana huhimizwa kujiepusha ya uhusiano utakao waletea athari hii. Haya yanasaidia kukabili mimba ya ujana na mimba isiyotarajiwa.
Q3: Mbona elimu ya jinsia na ngono ifunzwe mapema?
Elimu ya mapema kwa vijana ni muhimu kwa kusaidia yafuatayo:
- Kukinga watoto kudhulumiwa– endapo watoto wanafahamu mabo ya muhimu kuhusu maumbile yao, ni rahisi kukabili dhulumaza kijinsia katika jamii.
- Kuimarisha uhusiano na watu wengine– ni muhimu kuzingatia mawaidha haya ili kuwapa watoto na vijana mwongozo wa uaminifu kati yao na watu wakubwa kwa ufahamu wa maumbile yao na heshima yanayohitaji.
- Kuwaongoza kabla ya ujana– ni vyema kwaanda watoto/vijana katika mri mdogo yale ambayo watakabili katika ujana wao. Hili ni jambo la muhimu ili kukabili hisia za baadaye.
Q4: Ni jukumu la nani kuwafunza vijana kuhusu afya ya ngono na mfumo wa uzazi?
Vijana hukabiliana na watu tofauti katika maisha yao. Ni jukumu la jamii kunawiri uhusiano bora ili vijana wapate maarifa kutoka kwa watu wakubwa. Vile vile, wazazi kama walimu wa kwanza wana jukumu la kuanzisha mafunzo haya kisha walimu katika shule wanazo shiriki.
Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yana wajibu wa kutekeleza mifumo na mitaala ya kuwafunza vijana na kufadhili ufikivu wa mafunzo haya katika pembe zote.