Mimba isiyo kamili ni nini?
Mimba isiyo kamili hutokea wakati mwili wako haujaondoa kabisa mabaki ya ujauzito baada ya kutoa mimba kwa njia ya dawa (inayojulikana pia kama mimba ya kitabibu) au baada ya mimba kuharibika yenyewe (1, 2).
Dalili za mimba isiyo kamili
Ikiwa unadhani kuwa unaweza kuwa na mimba isiyo kamili, ni muhimu kuangalia dalili hizi za kimwili ambazo kawaida huhusishwa na hali hii:
- Maumivu ya chini ya tumbo au nyonga
- Kutokwa na damu ya wastani hadi nyingi ukeni; na
- Maumivu yanayosambaa hadi sehemu ya chini ya mgongo, sehemu za siri, au matako (1, 2).
Nifanye nini nikihisi mimba yangu haikutoka kikamilifu?
Ikiwa unahisi mimba yako haikutoka kikamilifu, ni bora kumwona mtoa huduma ya afya ambaye anaweza kuchunguza hali yako kwa usahihi. Ikiwa mimba isiyo kamili itathibitishwa, kuna chaguo kadhaa za matibabu, ikijumuisha matibabu ya upasuaji na ya dawa.
Mimba isiyo kamili hugunduliwaje?
Watoa huduma ya afya wanaweza kugundua mimba isiyo kamili kupitia kipimo cha damu au ultrasound. Kipimo cha damu hupima homoni inayoitwa human chorionic gonadotropin (hCG), ambayo huhusiana na ujauzito. Ikiwa mimba haikutoka kikamilifu, kiwango cha homoni hii huwa kidogo. Ultrasound hutumika kutafuta mabaki ya ujauzito ambayo bado yapo ndani ya mfuko wa uzazi (1).
Mimba isiyo kamili hutibiwaje?
Njia ya kutibu mimba isiyo kamili hutegemea hali yako ya kiafya na upendeleo wako binafsi. Kuna njia kuu 3 za kutibu mimba isiyo kamili:
- Ufuatiliaji wa kawaida: Wahudumu wa afya wanaweza kupendekeza kusubiri na kuona kama mwili utatoa mabaki ya ujauzito yenyewe bila kutumia dawa au upasuaji. Hii ni njia ya kawaida na salama, hasa katika hatua za mwanzo za ujauzito ambapo mwili mara nyingi huumaliza mchakato huu bila matatizo.
- Matibabu ya dawa: Hii inahusisha kutumia dawa ya kutoa mimba iitwayo misoprostol. Misoprostol hufanya kazi kwa kujifunga kwenye misuli na kusababisha mikazo kwenye mfuko wa uzazi, hivyo kusaidia mfuko wa uzazi kutoa yaliyomo (4).
- Matibabu ya upasuaji: Mara nyingi inaitwa Njia ya Kunyonya au Kufyonza, na hufanyika kwenye kliniki. Kwa kutumia Njia ya Kunyonya au Kufyonza, mtoa huduma ya afya atatumia kifaa cha kuvuta kwa upole kutoa yaliyomo ndani ya mfuko wa uzazi. Kuna aina mbili za matibabu ya upasuaji: Njia ya kunyonya au kufyonza na Njia ya Upanuaji na ukwanguaji kwa njia ya electoniki.Njia zote mbili zinatumia nguvu ya kuvuta kutoa tishu kutoka kwenye mfuko wa uzazi (3).
Shirika la Afya Duniani linapendekeza njia mbalimbali za matibabu kwa mimba zisizokamilika, lakini chaguo hizi hutegemea umri wa ujauzito.
Mimba chini ya wiki 14
Kwa mimba zilizo chini ya wiki 14, chaguo zifuatazo za matibabu zinaweza kutumika:
- Njia ya kunyonya au kufyonza na
- Matibabu ya dawa kwa kutumia misoprostol
Kuna njia mbili za kutumia misoprostol katika kutibu mimba isiyo kamili: ya kumeza na ya kuweka chini ya ulimi.Dawa ya kumeza ni ile unayokunywa na kumeza moja kwa moja.Dawa ya chini ya ulimi ni ile unayoweka chini ya ulimi na kuiacha iyeyuke au ukae nayo kwa muda.
Kiwango cha dawa kinatofautiana kulingana na njia ya utumiaji. Shirika la Afya Duniani inapendekeza kutumia aidha Mikrogramu 600 ya misoprostol kwa njia ya mdomo AU Miligramu 400 kwa njia ya Chini ya Ulimi (2).
Mimba ya wiki 14 au zaidi
Kwa mimba za wiki 14 au zaidi, Shirika La Afya Duniani inapendekeza matibabu ya dawa kwa kutumia misoprostol. Unaweza kurudia dozi ya Miligramu 400 ya misoprostol kila baada ya masaa matatu. Inapatikana kwa njia ya:Chini ya ulimi), Ukeni , ama Kati ya jino na shavu (2)
Nini cha kutarajia baada ya matibabu ya mimba isiyo kamili?
Baada ya matibabu ya mimba isiyo kamili, unaweza kupata kutokwa na damu isiyo ya kawaida au matone ya damu kwa hadi wiki mbili. Unaweza kutumia pedi kudhibiti na kufuatilia damu. Ikiwa umetumia misoprostol, tegemea kutokwa na damu nyingi kwa hadi siku nne.
Aidha, unaweza kupata maumivu ya tumbo chini kama dakika 30 baada ya kutumia misoprostol. Maumivu haya yanaweza kudumu kwa wiki chache. Hali hii inaweza kufanana na hedhi ya kawaida au kuwa kali zaidi. Hii hutokea kwa sababu mfuko wa uzazi unajirudisha katika ukubwa wake wa awali kabla ya ujauzito (3,5).
Misoprostol pia inaweza kusababisha athari nyingine kama vile homa na baridi. Homa haipaswi kudumu zaidi ya saa 24. Inaweza pia kusababisha athari kwenye mfumo wa chakula kama vile kichefuchefu, kutapika na kuharisha. Kichefuchefu na kutapika hutoweka kati ya saa 2 hadi 6. Kuharisha hupungua ndani ya siku moja. Hatimaye, misoprostol pia inaweza kusababisha vipele kwenye ngozi, ambavyo havipaswi kudumu zaidi ya saa chache (5).
Njia bora ya kupona baada ya matibabu ni kupumzika kadri iwezekanavyo. Hata hivyo, unaweza kurudi kwenye shughuli zako za kawaida siku inayofuata ikiwa utajisikia vizuri. Unaweza pia kutumia dawa za kupunguza maumivu kama ibuprofen (Advil) au acetaminophen (Tylenol). Daima fuata maelekezo ya matumizi kwenye kifungashio (3).


