Utoaji mimba ni utaratibu wa kawaida wa kimatibabu unaotumika duniani kote, hata hivyo, utaratibu huu haukubaliki sana katika jamii nyingi. Unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba umekuwa sababu kubwa inayo pelekea kuongeza idadi ya utoaji mimba usio salama duniani kote. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, wanawake 30 kati ya 100,000 hupoteza maisha kutokana na utoaji mimba usio salama. Takwimu hizi zimeenea zaidi katika nchi zinazoendelea. Hii pia ina maana kwamba watu wengi katika mazingira yenye vikwazo vya kisheria au katika mazingira ya rasilimali chache, hulazimika kugeukia utoaji mimba usio salama ambao una madhara makubwa na wakati mwingine kusababisha vifo.
Utoaji mimba ni utaratibu wa matibabu. Utaratibu huu hufanyika kwa kutumia dawa au kwa njia ya upasuaji ambao hufanyika kwa dhumuni la kuondoa ujauzito. Utoaji mimba unapofanywa kwa kutumia njia sahihi, huwa na ufanisi mkubwa na salama. Endapo tutakomesha unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba, watu watakuwa na imani zaidi ya kutafuta huduma za utoaji mimba kwa njia salama, na hivyo kupunguza kiwango cha vifo vinavyohusiana na utoaji mimba.
Unyanyapaa Dhidi ya Utoaji Mimba ni Nini?
Unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba hutokana na imani na mitazamo ya jamii kuhusu utoaji mimba. Ni dhana iliyo zoeleka kuwa utoaji mimba ni jambo baya kimaadili na halikubaliki katika jamii. Ingawa kila jamii ina aina fulani ya unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba usio salama, nchi nyingi zina dini, imani na tamaduni zinazozidisha unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba. Kwa mfano, dini nyingi zinapinga utoaji mimba na huona kuwa ni dhambi.
Baadhi ya mashirika yanayounga mkono maisha hueneza propaganda kuhusu utoaji mimba kwa kuchochea tafsiri hasi zinazohusiana na mimba za “kuchelewa” (late-term). Japokuwa wataalamu wa matibabu hawatumii misemo inayotumiwa na kikosi cha “pro-life”, wala hawana ufafanuzi kuhusu wakati ambapo mimba inachukuliwa kuwa imechelewa, hata hivyo hutumia lugha hii ya kudanganya ili kunyanyapaa utoaji mimba.
Ni Yapi Madhara ya Unyanyapaa Dhidi ya Utoaji Mimba?
Wanawake wanao hitaji kutoa mimba wako kinyume na maadili ya kitamaduni ambayo yanajumuisha wazo kwamba ngono inatumika tu kwa uzazi na kwamba wanapaswa kubaki safi kingono mpaka pale watakapo hitaji uzazi. Imani hizi za kuzuia ngono, huendeleza unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba hivyo kupelekea athari mbaya za ndani na nje. Madhara ya ndani ni yale anayopata mtu anayetaka kutoa mimba kutokana na mtazamo wa jamii kuhusu utoaji mimba. Athari hizi zinaweza kujumuisha hisia za aibu, hatia, wasiwasi, na huzuni. Hisia za kupinga utoaji mimba huelekea kuingizwa ndani, na zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiakili. Pia inaweza kuwa kikwazo kwa mtu ambaye anataka kutoa mimba na afya yake ya akili kwa kuwa uzoefu wao mara nyingi hunyamazishwa na jamii.
Katika jamii ndogo, pia kuna athari za nje ambazo zinaweza kutokea ikiwa wanawake watajadiliana kuhusu utoaji mimba. Kwa mfano, wanaweza kutengwa na familia zao, wenzi wao, au hata marafiki. Wanawake wengine pia hukabiliwa na ukosoaji na unyanyasaji. Inaweza hata kuwa hatari kujadili juu ya kutaka au kutoa mimba katika baadhi ya jamii kwa kuwa wanawake wengi wanaweza kukumbana na unyanyasaji, uchokozi, na ubaguzi. Kwa kweli, kumekuwa na waandamanaji wengi wanaounga mkono maisha ambao huwanyanyasa wanawake na watoa huduma za afya nje ya kliniki za utoaji mimba.
Katika nchi nyingi za Amerika ya Kusini, kumekuwa na mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika hivi karibuni ambayo yameruhusu utoaji-mimba katika mazingira fulani. Hata hivyo, licha ya sheria mpya, wanawake wengi bado wanakabiliwa na unyanyapaa. Kwa mfano, ingawa Uruguay iliharamisha utoaji mimba mwaka wa 2012, wanawake bado wanahisi kurudishwa nyuma na kubaguliwa na wataalamu wa afya miaka miwili baada ya sheria kubadilika.
Licha ya athari kwa wanawake, pia kuna athari za unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba kwa jamii.
Unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba huendeleza mawazo ya kizamani ya kanuni za kijinsia na kujieleza kwa jinsia ya kike. Majukumu haya ya kijinsia ni pamoja na wazo kwamba jukumu la mwanamke ni kuwa mama na kwamba wanawake wanahitaji kuwa wa kike na safi. Pia inaendeleza imani kwamba ngono inapaswa kuwa kati ya wanandoa tu kwa lengo la kupata watoto.
Je, Watoa Huduma za Utoaji Mimba na Kliniki Wanaathiriwaje na Unyanyapaa Dhidi ya Utoaji Mimba?
Katika utafiti wa kimataifa uliofanywa na safe2choose na Ipas, tulijaribu kufahamu uzoefu wa washirika na watoa huduma za utoaji mimba duniani kote. Ripoti hiyo ina takwimu za wazi za unyanyapaa unao wakabili watoa huduma za utoaji mimba. Mbali na unyanyapaa wa kijamii unaowakabili watoa huduma hao, ripoti hiyo ilibaini kuwa baadhi yao, kutegemea na eneo wanaloishi, pia wanakabiliwa na hofu ya jumla ya kuteswa au kukosa ulinzi wa kisheria katika jamii wanazo zihudumia. Baadhi waliripoti kwamba changamoto kubwa zaidi wanazokabiliana nazo ni mazingira ya uhasama, vikwazo vya kisheria, na woga wa kuteswa au kukosa ulinzi wa kisheria.
Madhara ya unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba si tu kwamba yanaathiri wanawake wanaotaka kutoa mimba, bali pia yanaathiri wahudumu wa afya wanaotoa dawa za utoaji mimba. Madaktari na wataalamu wengine wa afya mara nyingi huitwa majina ya kejeli na kuchukuliwa kuwa wenye dhambi katika nchi nyingi. Pia kumekuwa na matukio mengi ambapo waganga wanaotoa huduma ya kutoa mimba hushambuliwa na wakati mwingine kuuawa. Linapokuja suala la changamoto za utoaji mimba, ni muhimu kukumbuka kwamba watu wote wanao husika katika utoaji mimba huwa wanaathiriwa vibaya na unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba pia.
Kwa hivyo ingawa tunaweza kuona wazi athari za unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba kwa watoa huduma za afya, lazima tuelewe hii inaweza kumaanisha nini katika suala la mtoa huduma kujisikia salama na kulindwa vya kutosha kuweza kutekeleza majukumu yake kwa usalama bila hofu ya mateso, kejeli, na unyanyapaa. Watoa huduma za utoaji mimba wanaweza tu kutoa huduma kwa njia salama ikiwa wapo katika hali ambayo wanahisi maisha yao ni salama na jamii haitawahukumu kwa kutekeleza majukumu yao ya kutoa matibabu na kuokoa maisha ya watu wengi.
Je, Tunaweza Kufanya Nini Kuhusu Unyanyapaa Dhidi ya Utoaji Mimba?
Ingawa hakuna njia ya kutokomeza maramoja vizazi vinavyofanya unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba, bado kuna njia nyingi za kusaidia kuzuia unyanyapaa. Mashirika na wataalamu wa afya wanapo endelea kuelimisha umma, wanawake watawezeshwa zaidi kufanya maamuzi yao wenyewe kuhusu miili yao. Wale wanaoamini na kuacha unyanyapaa wanaweza pia kuanza kubadili mawazo yao kuhusu utoaji mimba mara tu wanaposikia ushahidi wa ukweli kuhusu hilo. Ki msingi, unyanyapaa ndio sababu kuu ya utoaji mimba usio salama ambao una athari mbaya.
Vikundi vya kisiasa vinavyounga mkono uchaguzi, mashirika na wanasiasa pia wanapaswa kuendelea kupinga kuharamishwa kwa utoaji mimba ili watu wengi zaidi waweze kupata huduma za utoaji mimba kwa njia salama. Kadiri utoaji mimba salama unavyozidi kuwa jambo la kawaida, watu watasikia visa zaidi kuhusu marafiki na wanafamilia waliotoa mimba kwa njia salama. Katika safe2choose, pia tunawahimiza watu kutoa visa vyao na kwakupitia visa vyao, wanaweza kujikomboa wenyewe na kuwakomboa wengine. Hii pia itasaidia kupunguza unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba kwa kuwa kutakuwa na watu wachache watakao endeleza unyanyapaa wa kitamaduni. Kuwasaidia wanawake wanao hitaji kutoa mimba pamoja na watoa huduma wa utoaji mimba kutasaidia kupunguza unyanyapaa dhidi ya utoaji mimba na hilo litapelekea wanawake kuwa salama na kusimamia afya zao za uzazi wakati wote.