Utoaji Mimba Nyumbani: Mambo 5 Unayopaswa Kuyajua

Mwanamke akisoma kuhusu utoaji mimba nyumbani kwenye simu yake, akiwa na kikombe cha chai.

Utoaji mimba nyumbani – pia hufahamika kama utoaji mimba kwa kutumia dawa, utoaji mimba wa kimatibabu, au utoaji mimba binafsi – unazidi kuwa maarufu miongoni mwa wanawake wanaotamani kutoa mimba. Utaratibu ni rahisi, hauhitaji upasuaji, na unaweza kufanywa mahali popote ambapo mtu anajisikia vizuri na salama.

Ili kutoa mwanga kuhusiana na utaratibu huu ambao ni salama na unaofaa, yafuatayo ni mambo 5 unayopaswa kuyajua kuhusu toaji mimba nyumbani.

1. Nini Maana ya Kutoa Mimba Nyumbani na Nani Anayeweza Kufanya Hivyo?

Utoaji mimba nyumbani (utoaji mimba kwa kutumia vidonge) kwa kawaida hujumuisha mchanganyiko wa dawa mbili zinazofanya kazi pamoja kufanikisha utoaji mimba. Dawa mbili zinazotumika ni Mifepristone na Misoprostol. Mifepristone hufanya kazi kwa kuzuia mtiririko wa progesterone – homoni muhimu inayosaidia kupata ujauzito. Misoprostol hufanya kazi kwa kusababisha maumivu na hatimaye kusafisha kizazi (uchafu hutoka kwa njia ya damu). Utoaji mimba kama matibabu pia unaweza kufanywa kwa kutumia Misoprostol pekee, lakini nivema zaidi kutumia dawa zote mbili pamoja. Kwa hakika, mchanganyiko wa Mifepristone na Misoprostol umeonekana kuwa bora zaidi kwani hufanikisha watumiaji 95 kati ya 100 kutoa mimba wakati matumizi ya Misoprostol peke hufanikisha watumiaji 85 kati ya 100 kuweza kutoa mimba kikamilifu.

Utoaji mimba kwa kutumia dawa ni utaratibu wa kawaida na salama wa kutoa mimba ndani ya miezi mitatu ya kwanza. Ili kuwa salama, utoaji mimba kwa kutumia dawa unaweza kufanywa kwa mimba yenye umri wa hadi wiki 13, au karibu miezi mitatu baada ya siku ya kwanza ya hedhi yako ya mwisho. Kwa mujibu wa Planned Parenthood, vidonge vya kutoa mimba vinafaa kwa asilimia 98 ikiwa una ujauzito wa hadi wiki nane, asilimia 96 hufaulu ikiwa una ujauzito wa kati ya wiki nane hadi tisa, na asilimia 93 ikiwa una ujauzito wa kati ya wiki tisa na 13. Baada ya wiki 13, upasuaji huhitajika ili kuweza kutoa mimba.

2. Nawezaje kupata vidonge vya kutoa mimba?

Sheria zinazo husiana na utoaji mimba kwa kutumia dawa, hutofautiana kati ya nchi moja na nyingine. Vidonge vya kutoa mimba vinapatikana katika nchi nyingi za Ulaya, Amerika Kaskazini, na Oceania. Katika mabara kama vile Afrika, Amerika ya Kusini, na Asia, upatikanaji wake unaweza kuwa na vikwazo zaidi. Mifepristone inaweza isipatikane lakini Misoprostol ni rahisi kupatikana. Kwa hakika, wakati Mifepristone hutumika kwa utoaji mimba tu, Misoprostol ina matumizi mengine ya kimatibabu mbali na kutoa mimba (kusababisha uchungu, kuzuia kuvuja damu baada ya kujifungua, matibabu ya vidonda vya tumbo, n.k). Ikiwa kuna ulazima, taasisi ya safe2choose inaweza kukuelekeza kwa mashirika ya kuaminika yanayoweza kukusaidia kupata vidonge vya utoaji mimba au kupata taarifa za msingi. Unaweza kuwasiliana nasi kwa barua pepe info@safe2choose.org.

3. Nitarajie nini na yapi ni madhara?

Wakati wa mchakato huo, madhara yanaweza kutokea kwa viwango tofauti. Baada ya kumeza kidonge cha kwanza cha Mifepristone, watu wengi hawapati madhara yoyote, lakini ni kawaida kuhisi kichefuchefu au kuanza kutokwa damu. Baada ya kumeza kidonge cha pili, kwa kawaida, seti ya Misoprostol 4, unaweza kuanza kutokwa na damu, na kuhisi maumivu ya tumbo yanayo lingana na maumivu ya hedhi ya kawaida. Unaweza pia kuhisi kichefuchefu na kupata maumivu makali ya tumbo na kutokwa na damu nyingi.

Mabonge makubwa ya tishu au mabonge ya damu yanaweza kutoka baada ya kumeza Misoprostol (mabonge yenye ukubwa wa limao, kwa mujibu wa Planned Parenthood), hasa kati ya wiki 9 na 13 za ujauzito. Kuvuja damu kunapaswa kuanza kupungua baada ya saa chache lakini kunaweza kuchukua muda mrefu zaidi. Maumivu ya tumbo yataendelea kwa siku moja au mbili na kupungua kadiri muda unavyo kwenda. Dawa ya Ibuprofen inaweza kusaidia kupunguza maumivu, pia aspirini inapaswa kuepukwa kwani inaweza kusababisha kutokwa na damu zaidi. Watu wengi hulinganisha utoaji mimba kwa kutumia dawa na hisia ya kuharibika kwa mimba.

Madhara mengine ni pamoja na kichefuchefu, kutapika, kuhara, kizunguzungu, uchovu, na homa ya wastani yenye hadi nyuzi joto 100. Ikitokea homa inapanda zaidi ya hapo, daktari anapaswa kuitwa mara moja. Uwezekano wa kupata maambukizi wakati wa utoaji mimba nyumbani ni mdogo sana lakini wanawake wanapaswa kuchukua tahadhari.

4. Je, utoaji mimba nyumbani ni salama?

Utoaji mimba nyumbani ni salama kabisa ikiwa utafanywa kwa usahihi. Mamilioni ya watu wametumia vidonge hivyo kwa usalama. Chini ya asilimia 1 ya watu wanaotoa mimba kwa kutumia dawa hupata madhara makubwa au mimba kuto toka vizuri. Ikiwa hali hii itatokea, wanawake wanaweza kushauriana na daktari au mshauri kuamua ikiwa watapaswa kutumia dawa zaidi, kujaribu tena nyumbani, au kutoa mimba kwa upasuaji ikiwa nchi yao inaruhusu.

5. Nitajisikiaje baada ya kutoa mimba?

Kupumzika ni muhimu baada ya utoaji mimba nyumbani. Kwa kawaida unaweza kurudi kazini, shuleni, au katika shughuli nyingine nyingi za kawaida siku inayofuata. Epuka kazi nzito au mazoezi. Pia unashauriwa kutumia kondomu au njia nyingine za kuzuia mimba kwani uwezekano wa kupata mimba hutokea ndani ya muda mfupi (siku 8 baada ya kutumia vidonge vya kutoa mimba).

Watu wengi hujisikia vizuri ndani ya siku moja au mbili, lakini kutokwa na damu kunaweza kudumu kwa wiki moja au zaidi baada ya kutoa mimba. Pia maumivu ya tumbo yanaweza kudumu kwa siku kadhaa.

Baada ya kutoa mimba, ni kawaida kabisa kupata hisia nyingi tofauti. Kila mtu huwa na uzoefu tofauti. Watu wengi wamefarijika na hawajutii uamuzi wao. Wengine wanaweza kuhisi huzuni, hatia, au majuto kwani pia wanapaswa kukabiliana na unyanyapaa mwingi kutoka katika jamii. Watu wengi hupata hisia hizi zote kwa nyakati tofauti.

Tuko hapa kukusaidia kutoa mimba ukiwa nyumbani

Watu wengi hujisikia vizuri zaidi ikiwa wana mtu wanayeweza kuzungumza naye baada ya kutoa mimba nyumbani. Lakini hata kama unadhani hakuna mtu maishani mwako unayeweza kuzungumza naye, hauko peke yako. Unaweza kuwasiliana na timu yetu ya washauri wa kike kwani daima ipo tayari kusikiliza kupitia barua pepe info@safe2choose.org.